Kutoka ENIAC hadi Kompyuta za kiganjani
ENIAC: Kompyuta ya Kwanza
Mapinduzi ya kweli yalianza takriban mwaka 1946 kwa kuzaliwa kwa ENIAC (Electronic Numerical Integrator and Computer). Hii ndiyo ilikuwa kompyuta ya kwanza kutengenezwa kielektroniki, na ilikuwa ajabu kwa wakati wake.
Uzito wake ulikuwa zaidi ya tani 27 – sawa na tembo wanne wa Kiafrika! Ilichukua nafasi ya chumba kizima, ikitumia maelfu ya vacuum tubes ili kufanya hesabu. Licha ya ukubwa huo, ENIAC ilifanya kazi kwa kasi ya ajabu, ikihesabu maelfu ya mahesabu kwa sekunde moja. Ilikuwa ni mwanzo, ikituonyesha uwezekano wa teknolojia ya kisasa, ingawa bado haikufikika kirahisi.

Mageuzi ya Transistor: Kompyuta Kuwa Ndogo na Zenye Nguvu
Mapinduzi ya pili yalikuja na uvumbuzi wa transistor mwishoni mwa miaka ya 1950. Transistor zilikuwa ndogo sana, zenye ufanisi zaidi, na zilitumia umeme kidogo kuliko vacuum tubes.
Hii ilileta enzi mpya ya kompyuta. Baada ya miaka michache, uvumbuzi wa Integrated Circuit (IC) au 'chip' uliruhusu mamilioni ya transistor kusinyaa na kuwekwa kwenye kipande kimoja cha silikoni. Hatua hii ilifanya kompyuta ziwe ndogo na zenye nguvu sana. Kompyuta kama desktop na mainframe zilianza kuwa ndogo na za bei nafuu, kuanza kuingia kwenye ofisi na, hatimaye, majumbani.

Zama za Kompyuta Binafsi (PCs) na Laptops
Kufikia miaka ya 1980 na 1990, teknolojia ilikuwa imeendelea kwa kasi. Kompyuta binafsi (Personal Computers – PCs) zikawa vifaa vya kawaida. Kisha zikaja laptops, kompyuta ambazo ungeweza kubeba. Chipu za kisasa ziliwezesha mashine hizi kuwa nyembamba, nyepesi, na bado zenye uwezo wa kushughulikia kazi ngumu. Leo, kompyuta hizi zenye nguvu ndogo (kama Macbooks, n.k.) ndizo tunazozitegemea.

Kuingia kwa Single Board Computers (SBCs)
Hata hivyo, kulikuwa na pengo. Licha ya kompyuta za kisasa kuwa na nguvu, zilikuwa na bei ya juu. Watu wa ubunifu, wanafunzi, na watengenezaji wa vifaa walihitaji jukwaa la majaribio lisilo na gharama kubwa.
Hapa ndipo Single Board Computers (SBCs) zilipoingia. Hizi ni kompyuta ndogo na zote zimejengwa kwenye bodi moja – CPU, RAM, na bandari zote za I/O. Ziliundwa mahsusi kuweka uwezo wa kuunda na kupanga (coding) mikononi mwa kila mtu kwa gharama nafuu. Kiongozi mkuu wa mapinduzi haya ni Raspberry Pi, kompyuta ndogo yenye ukubwa wa kadi ya benki
